Advertisemet

.

Sunday, 4 May 2014

WANAWAKE KUTONYONYESHA WANAUME WALAUMIWE PIA.


Mifumo ya kuendesha maisha yetu siku hizi imebadilika. Mtu ukirudi nyuma miaka 15 iliyopita unayaona mabadiliko hayo kwa wazi kabisa.

Tulikuwa hatuna mashine za kutolea fedha sasa mtu kukwambia kwamba anakwenda kuchukua fedha kwenye ‘ATM’ ni kitu cha kawaida, hata kama anadanganya. Tunanunua umeme na huduma nyinginezo tukiwa nyumbani kupitia simu zetu.

Tukianza kuorodhesha moja, moja tutamaliza sehemu yote ya makala haya na tusiyamalize. Kweli ni mengi mno. Pamoja na mabadiliko yote hayo, bado kuna mambo yasiyokubalika katika maisha ya mwanadamu.

Hata hivyo, leo ningependa tuzungumzie uhitaji wa chakula katika mwili wa binadamu. Pamoja na mabadiliko yote hayo bado binadamu anahitaji chakula, tena kwa viwango vya virutubisho vinavyotakiwa.

Hakuna teknolojia iliyoingia ikatoa uthibitisho kwamba binadamu sasa hana haja ya kupata wanga, protini na vitu kama hivyo ndani ya mwili wake.

Hata Mungu aliyetuumba alihakikisha tunapata virutubisho hivyo kupitia vyakula mbalimbali vinavyopatikana katika maeneo yote.

Mungu alituumbia pia mfumo wa kupata aina hiyo ya virutubisho pale tunapozaliwa. Akamjali mwanamke kuwa na matiti kifuani pake na kumjaza maziwa tayari kwa ajili ya mtoto anayezaliwa ili iwe lishe yake mpaka hapo atakapoweza kula chakula kingine.

Hakuna teknolojia iliyoweza kutengeneza chakula kinachozidi hiki kilichoandaliwa na Mungu kwa ajili ya mtoto. Chakula hiki ni bora na wataalamu wanasema mtoto anastahili kulishwa kwa miezi sita bila kuchanganywa na chakula kingine kwa afya bora ya mtoto.

Pamoja na uzuri wa chakula hiki kilichobarikiwa na Mungu, limezuka balaa kwa wanawake kuwanyima watoto wao chakula hiki muhimu.

Wanawake wa leo hawataki kunyonyesha. Inasikitisha kuona kwamba mtoto anakataliwa kula kile chakula bora ambacho Mungu alikiwekea virutubisho vyote anavyostahili kuvipata mtoto kwa ajili ya kukua kwake kiakili na kimwili, pamoja na kumpa kinga dhidi ya maradhi.

Wanaokataa kuwanyonyesha watoto wao, wengi ni wanawake wasomi, wenye uelewa mzuri wa chakula kimfaacho mtoto mchanga.

Swali linabaki ni je, kitu gani kinawafanya wasinyonyeshe pamoja na uelewa wote huo? Hili ndilo la kuliangalia katika makala haya.

Kwa upande mmoja ningependa niwalaumu wanaume. Ndiyo, wanaume, hasa waliooa na kuwazalisha wanawake hao wenye kuwanyima watoto maziwa yao yaliyo bora kwa afya.

Wanaume wengi wanawadharau wake zao pale matiti ‘yanapodondoka’ baada ya kuanza kunyonyesha. Tena wengine kwa kebehi kabisa husema, “nani anataka hizo kanda mbili”. Anamwacha mkewe na kwenda kutafuta wale ambao hawajaanza kunyonyesha.

Haijaanza leo kebehi hiyo, sasa akinamama vijana, wanaona njia ya kusitisha kebehi hiyo ni kuendelea kuhifadhi matiti yao kwa kutonyonyesha.

Sina hakika kama hiyo ni dawa ya kudumu au la kwa matiti kutoanguka. Kinachoniumiza ni kwamba katika jitihada hizi za kutotaka matiti yaanguke anayeumia ni mtoto ambaye wala hakuwaomba wazazi hao kumleta duniani. Cha ajabu, asingepatikana, ungeona namna ambavyo wangehaha kumtafuta. Mwingine angekimbilia kwenye huduma za kiroho na nyinginezo, mwanamke angekula dawa zote zinazopatikana zenye kumpa tumaini la kupata mtoto.

Mwanaume naye ungesikia ameamua kuzaa na mwanamke mwingine kwa kuwa mke hapati mtoto. Hii inatuonyesha kwamba mtoto anatakiwa, lakini eti asisababishe matiti ya mama kudondoka. Haya ni maajabu, yaani watu wanataka wapate yote kwa pamoja yaani wapate mtoto na matiti yasidondoke.

Kama mwanamke unatimiza wajibu wako hilo haliwezekani. Ama usizae na ukae na matiti yako yaliyosimama mpaka uzeeni kisha ujilaani mwenyewe kwa kukosa mtoto, au ukubali kupata mtoto na uwajibike kwake apate afya njema lakini kwa kufanya hivyo ukubali matiti yadondoke.

Enyi wanaume, waonyesheni wanawake hawa kwamba mtaendelea kuwapenda hata kama matiti yao yatadondoka kwa kunyonyesha ili kukinusuru kizazi kijacho.

Kwa kushiriki katika kuendeleza uzao wa binadamu, mjue mna wajibu mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu kujenga kizazi kitakachokuwa na afya ili waweze kumudu mazingira ya dunia hii kwa ufanisi unaotarajiwa.

Siyo kuleta kizazi ambacho kitakuwa na dosari za kiafya kwa sababu tu ya starehe ambazo ni za muda mfupi. Hivi unakuwa na raha gani mwanaume kwa kuendelea kumwona mkewe ana matiti yaliyosimama, lakini mwanao ana matatizo ya kiafya kwa sababu tu hakupata lishe inayostahili ya maziwa ya mama alipozaliwa?

Siamini kama kuna mwanaume ambaye angependa hali hiyo. Kila baba angependa kuona watoto wake wanakuwa na afya bora.

Kama hayo ni matumaini ya kila baba, basi baba huyo akubali kwamba njia mojawapo ya kuhakikisha watoto wake wanapata afya njema ni kuhakikisha kuwa wananyonyeshwa, lakini kunyonyesha kunaendeana na matiti ya mkeo kuporomoka hivyo likubali hilo.

Usimwone mkeo kama ana kasoro kwa sababu ya kunyonyesha, ukifanya hivyo utakuwa umechangia katika kuwafanya akinamama waone kama kunyonyesha ni kitendo kinachowafanya waume zao wawakimbie, hivyo kwao kunyonyesha ni kitendo cha kuogopa kama ukoma.

Pamoja na kwamba leo nilikuwa na haja ya kusema na waume zetu, lakini hebu akinamama tulitafakari hili. Eti tunaacha kunyonyesha kwa sababu wanaume watatukimbia. Hii inasikitisha sana.

Hebu fumba macho yako mwanamke, hebu fikiria uchungu ulioupata wakati wa kumleta mtoto huyo duniani; ule uchungu utaulinganisha na nini hata baadaye, uone mtoto huyo anastahili kupewa lishe duni isiyofaa ndani ya mwili wake kwa sababu tu ya furaha ya muda?

Kwa nini hatupendi kuukumbuka uchungu huo na kuwa na uchungu na watoto hao waliotokana na uchungu huo? Si tunaambizana kwamba kwa uchungu tulioupata ukisikia mtoto analia nje wewe huku ndani ule uchungu unarudi tena?

Sasa katika ufahamu wako, weka picha ya mtoto wako akiwa ameathirika kwa kukosa maziwa yako halafu ule uchungu utarudi. Ukirudi utaona umuhimu wa kumnyonyesha mwanao. Mnyonyeshe mwanao na Mungu atakubariki hata katika ndoa yako.

No comments:

Post a Comment

 
Don't Forget To Join US In MalikiaTz Community
×
bloggerWidget