Ujenzi wa Sekondari za Kata katika mikoa mbalimbali umesogeza huduma za elimu kwa baadhi ya maeneo. Ipo mikoa ambayo awali ilikuwa na shule chache za sekondari hali ambayo ilifanya wanafunzi wachache kupata fursa ya kujiunga na sekondari. Kwa sasa hali si hivyo tena, mikoa mingi imeongeza idadi ya shule hizo licha ya changamoto kibao inazozikabili shule hizi.
Zipo baadhi ya shule za sekondari zimejengwa mbali kidogo na makazi ya wahitaji kitendo ambacho huwalazimu wanafunzi kutembea muda mrefu asubuhi wakielekea shuleni na baadaye jioni wakirejea nyumbani, hali ambayo ni changamoto kwa wengi wao.
Hata hivyo baadhi ya maeneo shule hizo zimejengwa mbali zaidi na makazi ya watu kutokana na kile kuhudumia vijiji ama vitatu hadi vinne, na hazina mabweni jambo ambalo wanafunzi wanashindwa kuvumilia umbali uliopo kutoka kijiji kimoja hadi kingine hivyo kutafuta mbinu mbadala ya kusogea jirani na shule wanazokuwa wamepangiwa.
Wanafunzi wanaamua kutafuta vyumba vilivyopo jirani na maeneo ya shule walizopangiwa na hivyo kupanga (kukodi chumba). Wenyewe vyumba hivi huviita mageto. Vyumba hivi huwa vidogo na vingine mithili ya vibanda, ambapo bei huwa ya chini zaidi kwa mwezi. Wanafunzi wengine huamua kujikusanya wawili ama zaidi na kuishi pamoja kwenye geto ili kupunguza gharama.
Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto baadhi ya maeneo aina hii ya maisha ya wanafunzi ni kitu cha kawaida. Wanafunzi wameamua kupanga kwenye mageto (vyumba mitaani) na kuishi kwa makundi huku wakikabiliwa na changamoto lukuki zinazohatarisha safari yao ya elimu ya sekondari.
Mbwambo Conrad ni Mkazi wa Kata ya Bungu wilayani Lushoto, eneo ambalo lina idadi kubwa ya wanafunzi waliopanga kutoka vijiji vya mbali huku wakihudhuria masomo yao ya sekondari. Anasema eneo hilo kuna wanafunzi wengi ambao wametoka vijiji vya mbali na wamepanga jirsni na shule kwenye kata hiyo kuhudhuria masomo.
Anasema wanafunzi hao wamepangiwa na wazazi wao ili waweze kuhudhuria masomo yao kuepuka umbali wanaotoka kwenye vijiji vyao. "Wanafunzi hawa wamepanga katika baadi ya vyumba na wanaishi kwa tabu sana...wengi wanaingia katika majaribu kutokana na aina ya maisha wanayoishi," anasema Mzee Conrad.
Anasema wavulana wengi huishia kuwa wahuni maana uangalizi wa wazazi hawana, mara nyingi utawakuta wamekaa vikundi kwa vikundi nyakati za jioni hadi usiku unaweza kufikiri sio wanafunzi. Wanachelewa kulala muda mwingi wanazunguka kwenye majumba ya sinema (vibanda vinavyo onesha picha za video) hivyo wanaishi kwa kujitawala utazani si wanafunzi.
Willson N'gwamizi ni Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muungui wilayani Lushoto, anasema licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali katika shule hiyo suala la wanafunzi kuishi kwenye mageto ni changamoto kubwa kwa shule kwani linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma. Anasema wanafunzi hulazimika kuishi katika vyumba hivyo vya kupanga kutokana na shule nyingi za kata zilizojengwa kutokuwa na mabweni huku zikichukua wanafunzi kutoka vijiji vya mbali.
"Kifupi suala la wanafunzi kuishi katika mageto linaathiri maendeleo ya shule kitaaluma...wanafunzi hawa wanapoishi huko hukosa usimamizi wa wazazi na wengine hata hela ya kumudu maisha hayo huwa ni tatizo maana wanatoka vijiji vya mbali na uwezo wa familia zao wakati mwingine hushindwa kuwatimizia mahitaji yote," anasema N'gwamizi.
Anasema kutokana na uhuru huo wa kukaa kwenye mageto wanafunzi wengine hutoroka na kwenda kufanya vibarua kwenye mashamba ya chai na sehemu nyingine wasichana nao huwa huru zaidi kitendo ambacho hushindwa kukabiliana na changamoto za vishawishi mitaani.
"Ukizunguka katika baadhi ya kata unaweza kukuta wanafunzi wa kidato cha pili wamepanga kwenye chumba kimoja, ndani ya chumba hicho wapo wawili hadi watatu...wengine wanatoka katika familia duni hawapewi mahitaji ya kutosha, wengine hujikuta wanashawishika na kuingia mitaani na kujikuta wanakatizwa masomo kwa kutiwa ujauzito," anasema.
"Kwa kweli mageto ni tatizo, wapo baadhi ya walimu hujitahidi kuwafuatilia huko wanakoishi ili kuhakikisha wanajenga nidhamu ya kiuanafunzi, hata hivyo zoezi hili bado ni changamoto maana na walimu wamejikuta wakikaa mbali na shule kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu jambo ambalo ni tatizo pia," anasema mwalimu huyo.
Suala la ukosefu wa mabweni kwa shule za kata na kuwalazimu wanafunzi kupanga mitaani (mageto) halipo kwa wilaya ya Lushoto pekee. Wilaya ya Handeni nayo inakabiliwa na changamoto hiyo ya wanafunzi kupanga uswahilini wenyewe karibu na shule walizopangiwa.








No comments:
Post a Comment