Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya Balozi wa Kampeni ya Simama kwa ajili ya Mwanamke wa Afrika “Stand for African Mother campaign” kutokana na kujitoa kwake kuwahamasisha wake wa marais wa Afrika kusimama na kupigania haki za mama na mtoto.
Hafla fupi ya kukabidhi tuzo hiyo iliyotolewa na taasisi inayoshughulika na masuala ya Afya Afrika (Amref) ilifanyika Ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) zilizopo jijini Dar es Salaam.
Akiongea kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Dk. Festus Ilako alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi anayoifanya kuhakikisha vifo vya wajawazito na watoto vinapungua nchini.
“Tangu kuzinduliwa kampeni hii mwaka 2012, tumefanikiwa kusomesha wakunga 250. Hii ni karibu na asilimia 10 ya wakunga ambao wanatakiwa kusomeshwa katika kampeni hii.
Changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha za kutosha za kuwasomesha wakunga hawa, lakini naamini ifikapo mwaka 2016 malengo yetu yatatimia,” alisema Dk. Ilako.
Alisema mkunga mmoja anaweza kuwahudumia wanawake 5,000 kwa mwaka, kama watu wataweza kulipia mafunzo ya wakunga idadi yao itaongezeka na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wama, aliwashukuru Amref kwa tuzo waliyompatia na kusema kuwa siyo kama yeye ni hodari, bali ni kutokana na kujitoa kwake kushiriki na kupigania mambo mbalimbali yanayowahusu wanawake.
Mama Kikwete alisema: “Ukimwezesha mwanamke mmoja umeiwezesha familia nzima, pia mwanamke akiamua kuiinua au kutoiinua familia yake anaweza kufanya, hivyo jambo la muhimu ni kumsaidia ili aweze kupata elimu”.
Mama Kikwete aliwahimiza wake wa marais wa Afrika kuunga mkono kampeni ya Amref kuwasomesha wakunga 15,000 barani Afrika ili kupata wataalamu wengi zaidi watakaohudumia wajawazito wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza vifo vyao na vya watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.







No comments:
Post a Comment