Advertisemet

.

Tuesday, 15 April 2014

WANAWAKE WAJITOKEZA KWA WINGI KUPEWA SEMINA YA UZAZI WA MPANGO MKOANI DODOMA


 Watoa huduma wa PSI Tanzania wakiendesha zoezi la upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi  katika jukwaa la Familia Kitchen Party Gala 2014 iliyofanyika katika ukumbi wa kilimani  mjini  Dodoma.


Baadhi ya wanawake wakijisajili kabla ya kuingia katika Familia Kitchen Party Gala 2014 ambapo wanawake zaidi ya 300 walijumuika na kuhamasisha kushiriki katika zoezi la upimaji wa afya zao ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi na ukimwi.


Mwanzilishi wa jukwaa la Familia kitchen Party Gala 2014 Bi Vida Mndolwa akizungumza na wanawake waliohudhuria shughuli hiyo.


           Mwanamuziki wa kike wa hapa nchini Shilole akitumbuiza  katika onesho hilo


       Baadhi ya wanawake waliojitokeza katika jukwaa la Familia kitchen party mjini Dodoma.

Wanawake zaidi ya 300  wamejitokeza kupewa semina ya uzazi wa mpango, saratani ya shingo ya kizazi na elimu kuhusu ugonjwa wa Ukimwi iliyoandaliwa na Shirika linalotoa Elimu ya Afya la PSI Tanzania mjini Dodoma.

Mbali ya kushiriki katika semina hiyo, wanawake 90 walipima afya zao papo hapo baada ya kupata elimu, huku waandaaji wakisema uelewa mdogo ni kiini kikubwa cha wanawake kushindwa kupima afya zao ili kujitambua.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa semina hiyo, Meneja wa Huduma ya Uzazi wa Mpango wa PSI, Catherine Paul alisema bado uelewa kuhusu uzazi, saratani ya shingo ya kizazi, Ukimwi, malezi ya watoto ni tatizo kwa wanawake wa mijini na vijijini.

Kwa kweli mwitikio umekuwa mkubwa kuliko hata vile tulivyotarajia.Kama inavyofahamika ugonjwa wa saratani  ya shingo ya kizazi hivi sasa ni tishio kubwa na takwimu zinaeleza kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki alisema.

Leo tunashuhudia na kufurahi kuona kuwa wanawake hawa zaidi ya 300 wamekutana hapa ili kubadilishana mawazo na kupata elimu kwa mambo yanayowahusu hatua itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kubadili mifumo yao ya maisha baada ya kujitambua, alisema.

Kwa upande mwingine Mratibu wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto, Khadija Ameir alisema PSI imekuwa inatoa elimu kuhusu masuala hayo katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini kwa lengo la kumkomboa mwanamke na kustawisha maisha yake.

Alisema katika maeneo ya vijijini Shirika hilo limekuwa likiendesha kampeni ya nyumba kwa nyumba ili kuwafikai wanawake na kuwapa elimu kuhusu uzazi wa mpango, saratani  ya shingo ya kizazi, Ukimwi na malezi ya Mama na Mtoto, hatua ambayo imeongeza idadi ya wanawake ambao sasa wanatambua  kuhusu afya ya uzazi.

Ikumbuke kwamba PSI inawatumia wataalamu katika kufikisha elimu hii kwa wanawake hatua ambayo imesaidia kupunguza idadi ya vifo vya wanawake kutokana na masuala ya uzazi, Ukimwi na hata saratani ya shingo ya kizazi, huku pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikipungua, alisema Ameir.

Akizungumza Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Asasi ya Women in Balance (Mizania ya Wanawake), Vida Mndolwa alisema mwitikio wa wanawake katika kujitokeza kupata elimu wa afya ya uzazi, Ukimwi na saratani ya shingo ya kizazi umekuwa mkubwa kila mahala ambapo wanafika kutoa elimu hiyo.

Kama mnavyoona hapa Dodoma mwitikio umekuwa ni mkubwa sana na tunashukuru kuona wanawake wamejitokeza ili kupata fursa ya kukutana na wataalamu wa huduma za afya suala ambalo litaongeza uwezekano wa wao kujitambua na kuwa na maisha yaliyo bora na salama, alisema Mndolwa.

Mmoja wa washiriki Mwajuma Othman Mtuli alisema, Ni zaidi ya elimu, ni zaidi ya burudani, ni zaidi ya mafunzo. Kwa kweli semina hii imetusaidia kufahamu kuhusu kujua umuhimu wa malezi ya watoto, kutunza ndoa na hata ujasiriamali na hivyo tunaishukuru sana PSI kwa mafunzo haya.

No comments:

Post a Comment

 
Don't Forget To Join US In MalikiaTz Community
×
bloggerWidget